Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali imehimzwa kuingilia kati swala la kutibu eneo la Owino Uhuru, bunge la Jomvu kufuatia kuathirika na chembechembe za simu ya vyuma aina ya Lead kwa muda wa miaka mingi.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kupiginia haki za kimazingira la ‘Centre for Justice and Environment Action’ Bi Phyllis Omido, amesema kwamba idadi ya wakaazi wa eneo hilo wameathirika na sumu hiyo ya vyuma huku wengine wakiaga dunia.

Akizungumza mjini Mombasa na wanahabari siku ya Jumatano, Omido alisema kwamba kuna haja ya serikali kuingilia kati swala hilo na kuwasaidia wakaazi wa eneo hilo kwa kuwafanyia utafiti na kubaini viwango vya chembechembe ya sumu ya vyuma iliyo miilini mwao na kuwapa tiba maalum.

Amehoji kuwa shirika hilo halina uwezo wa kufanya utafiti zaidi mbali kwa ushirikiano na wadau mbalimbali pamoja na serikali kwa kiwango kikubwa wataokoa maisha ya wakaazi kutokana na kuenea kwa chembechembe za sumu hiyo.

"Hatuwezi kufanya utafiti sisi wenyewe tukamaliza, tunahitaji serikali ya kaunti na kuu kuingilia kati swala hili tusipoteze watu wetu wa Owino Uhuru, sisi tumejaribu sana kama shirika lakini kwa ushirikiano tutafaulu," alisema Omido. 

Mwanaharakati huyo ameyadokeza hayo huku utafiti uliyofanywa hapo awali ukibaini kuwa zaidi ya wakaazi 3,000 wameathirika na chembechembe za sumu hiyo tangu kampuni iliyokuwa ikitengeza vyuma kwa kutumia madini ya Lead kusitisha shughuli zao.