Viongozi mbalimbali katika kaunti ndogo ya Rabai wamezitaka serikali za kaunti kanda ya Pwani kushirikiana na serikali kuu ili kujenga shule zaidi za wanafunzi wanaoishi na ulemavu wakisema kuwa kwa sasa idadi ya wanafunzi hao inazidi kuongezeka ilihali shule hizo hazijaongezwa kwa kipindi kirefu.
Akizungumza hii leo katika mkutano uliowaleta pamoja washikadau mbalimbai katika sekta ya elimu katika kaunti ndogo ya Rabai, mkurugenzi mkuu wa elimu katika kaunti ya Kilifi Dickson Ole Keis amesema kuwa serikali inafaa kuwekeza zaidi katika utoaji wa huduma za masomo kwa wanafunzi wanaoishi na ulemavu kama vile wasiokuwa na uwezo wa kuona, kusikia na hata kutembea akisema wao pia wanahaki ya kupata elimu bora ambayo itakuwa msingi katika maisha yao.
Dickson amesema kuwa wanafunzi hao huwa werevu kiasi cha kufaulu katika mitihani yao ila jambo linalowafanya kubaki nyuma ni ukosefu wa vifaa vya kutosha katika shule wanakosomea na hata uhaba wa shule za kutosha jamba ambalo anasema ni kinyume cha sheria za hapa nchini kwani kila mmoja anapaswa kupata elimu sawia na mwenziwe pasi kubaguliwa.
Kwa upande wake mbunge wa kaloleni Gunga Mwinga ambaye ujumbe wake ulisomwa na msaidizi wake, ametoa wito kwa serikali kutengea sekta ya elimu fedha za kutosha katika mwaka wa fedha ujao ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata huduma za elimu pasi na ugumu wowote kama ilivyokuwa hapo awali.
Gunga katika taarifa yake amesema fedha za ustawishaji wa maeneo bunge katika eneo bunge lake zitatumika kumnusuru mtoto mlemavu ambaye amekuwa akiachwa nyumbani pasi kufika shuleni kupata elimu kwa misingi ya kutoweza kutembea wala kutoweza kuona, kuongea miongoni mwa ulemavu mwengine.
Aidha wazazi waliohudhuria mkutano huo wametakiwa kutowafungia wanawao majumbani bali kuwapeleka katika shule za kawaida wale wanaoweza kuongea huku serikali ikishuhulikia uhahaba wa shule za wanafunzi hao.
Hata hivyo kwa upande wao wazazi wamesema wanawao wamekuwa wakibaguliwa kila wanapowapeleka shuleni jambo ambalo wanasema limepelekea wao kutokuwa na imani na baadhi ya walimu na hata wanafunzi wengine ambao huwadharau wanawao.
Aidha wametoa wito kwa serikali kutoa mwelekeo mwafaka wa namna watakavyowasaidia wanawao ili nao wapate elimu.