Shinikizo zazidi kutolewa kwa serikali kuu kuongeza safari za ndege za kimataifa katika Uwanja wa ndege wa Moi, Mjini Mombasa.
Hatua hiyo inanuia kuongeza idadi ya watalii wanaozuru ukanda wa Pwani.
Akizungumza kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, mwenyekiti wa chama cha watalii nchini Mohammed Hersi, alisema hatua hiyo itasaidia katika kuikuza sekta ya utalii, hali itakayopiga jeki uchumi wa nchi vile vile.
Hersi alisema kuwa serikali inapaswa kuangazia swala hilo, kwani Kaunti ya Mombasa na ukanda mzima wa Pwani, ni miongoni mwa maeneo mbalimbali nchini yanayotegemea utalii katika ukuaji wake wa kiuchumi.
Wakati huo huo, Hersi ameongezea kuwa ni sharti mikakati mwafaka zaidi kuwekwa, ili kuwavutia watalii hasa ikizingatiwa kwamba msimu wa sherehe unakaribia, na sekta hiyo inalenga kuvuna zaidi kutokana na ongezeko la watalii mwezi Disemba.
Kwa upande wake, Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho aliahidi kushirikiana na wadau katika sekta ya utalii.
Joho alisema kwamba viwango vya utalii katika Kaunti ya Mombasa na kote Pwani, vinaendelea kuimarika baada ya kupitia hali ngumu ya msukosuko wa kiusalama katika miaka ya hivi majuzi.