Naibu wa Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Kutetea Maslahi ya Wafanyikazi nchini (COTU) Benson Okwaro, amewataka wanasiasa humu nchini wasitishe mjadala kuhusiana na pendekezo la kutaka kuiondoa Kenya kutoka mkataba wa Roma, uliounda mahakama ya kimataifa ya ICC.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza katika Chuo cha Leba cha Tom Mboya jijini Kisumu siku ya Jumatatu, Okwaro alipendekeza ushirikiano kati ya serikali ya Kenya na mahakama hiyo, akisema Wakenya wengi wangali wana matumaini katika mahakama hiyo.

“Mimi ukiniuliza nitakuambia kuwa tungali tunaihitaji ICC ili kuzuia uwezekano wa kutokea kwa ghasia katika taifa hili. Serikali yetu inafaa iunge mkono ICC au iweke mikakati ya kuiwezesha idara ya mahakama humu nchini kushughulikia kesi zinazohusiana na machafuko ya uchaguzi,” alisema kiongozi huyo wa COTU.

Okwaro alisema kuwa hatua ya ICC kufutilia mbali kesi dhidi ya Naibu wa Rais William Ruto na mwanahabari Joshua Sang hivi maajuzi, ni ishara tosha kuwa mahakama hiyo haikua na nia ya kuwakandamiza Wakenya hao, bali inazingatia ushahidi.

“Kesi dhidi ya Ruto na Sang ilifutiliwa mbali kwa sababu ya ukosefu wa ushahidi. Hiyo inaamanisha kuwa majaji wa ICC walifanya uamuzi kulingana na ushahidi, na wala sio kwa lengo la kuwakandamiza washtakiwa,” alisema Okwaro.

Alisisitiza kuhusu haja ya wanasiasa kupunguza cheche za maneno kuhusu kesi za ICC, akiwahimiza kuwapatanisha Wakenya.