Watu wanaoishi na ulemavu katika Kaunti ya Mombasa wamesema kuwa wanakumbwa na changamoto kubwa kutokana na uhaba wa watu wanoweza kutumia lugha ishara.
Makundi hayo ya watu wanaoishi na ulemavu yalisema kuwa serikali inafaa kuzingatia zaidi swala hilo kwani watu wenye ulemavu wa kusikia wamekuwa wakikosa huduma nyingi kutokana na changamoto ya mawasiliano.
Wakiongea katika kikao kilichowaleta pamoja walemavu mjini Mombasa siku ya Jumatano, washirikishi kutoka makundi mbalimbali ya walemavu walitoa wito kwa serikali kuwasajili watu zaidi katika masomo hayo muhimu.
Mwakilishi wa shirika la kitaifa la kushughulikia walemavu NCPWDS tawi la Mombasa Bi Sarah Ayiecho, alisema kwamba serikali imetoa mafunzo kwa zaidi ya watu 50 katika kaunti hiyo.
Ayiecho aliongeza kwamba serikali imetenga zaidi ya shilingi milioni tano kwa mpango huo huku wakilenga ofisi muhimu za umma.
“Tumetoa mafunzo kwa wauguzi hospitalini, maafisa wa polisi, miongoni mwa maafisa wengine katika eneo hili na bado mpango huo unaendelea,”alisema Bi Ayiecho
Watu wenye ulemavu wa kusikia mara nyingi hupitia changamoto ya mawasiliano kila wanapozuru ofisi za umma kutafuta huduma.
Hii inatokana na kuwepo kwa maafisa wachache wanaohudumu katika afisi hizo walio na ufahamu wa lugha ishara.