Serikali kuu na ile ya Kaunti ya Mombasa zimetakiwa kubuni mikakati mwafaka ya kuwasaidia vijana wenye nia ya kujinasua kutokana na utumizi wa dawa za kulevya ili kuona kwamba wanapata mbinu za kujikimu kimaisha.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumanne katika kongamano la hamasa, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reachout Centre Trust, Taib Abdulrahman alisema kwamba vijana wengi wanaojinasua kutoka kwa janga hilo hukosa mbinu ya kuanza maisha na hivyo basi kupelekea wengi wao kurejea katika utumizi wa mihadarati.

Abdulrahman alipendekeza serikali kuu na ile ya Kaunti ya Mombasa kutenga ajira zitakazopewa vijana hao ili kuzuia kupata msukumo wa kurejelea mihadarati.

Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia pakubwa vijana wengi kujihusisha na maswala muhimu ya kimaendeleo.

"Tunaihimiza serikali kuu na ya Kaunti ya Mombasa kuwatengea ajira vijana wanaonasuliwa kutoka kwa mihadarati ili kuwawezesha kujikimu kimaisha na kujitenga na uovu huo,” alisema Abdulrahman.

Mwanaharakati huyo aliwarai wazazi kuhakikisha kuwa wanawapokea vijana wao pindi wanaporejea nyumbani baada ya kupata matibabu maalum, kwa kusema kuwa wao pia ni kati ya jamii.