Mwenyekiti wa Maendeleo ya Wanawake katika eneo bunge la Mvita Amina Hamisi ameitaka serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wazazi wanaowabaka wanao na kuchangia ongezeko la mimba za mapema.
Kwenye mahojiano na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Jumatano, Hamisi alisema kuwa mara nyingi hali hiyo huchangiwa na baadhi ya wazazi wanaowapeleka watoto wao kufanya kazi za nyumbani na kupachikwa mimba na waajiri wao.
Alisema kuwa hali hiyo inachangia watoto wengi wanaozaliwa kuishia kurandaranda mtaani.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa iwapo serikali itaweka sheria kali dhidi ya wazazi na waajiri wanao wanabaka watoto, hatua hiyo itapunguza dhulma za kijinsia na watoto watapata fursa ya kusoma na kufanikisha malengo yao katika siku za usoni.
"Tunaitaka serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria watu kama hao ili kulinda watoto wetu wa kike na kuhakikisha kuwa wanasonga mbele kimasomo,” alisema Hamisi.
Wakati huo huo, amewataka wanaharakati kushirikiana na kuwalinda watoto wa kike waliotengwa na familia zao pamoja na mayatima ili kuwawezesha kusonga mbele na kupiga vita dhulma hizo.