Wito umezidi kutolewa kwa serikali kuwapa machifu na viongozi wa Nyumba Kumi bunduki ili kuwawezesha kujilinda dhidi ya kuvamiwa.
Haya yanajiri baada ya viongozi watatu wa Nyumba Kumi kuuawa katika Kaunti ya Kwale, huku mwingine mmoja akiuawa katika Kaunti ya Lamu.
Mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Lamu Shakilla Abdalla ametoa wito kwa serikali kuwapa machifu silaha hasaa wanaohudumu katika maeneo yanayokumbwa na uraibu wa dawa za kulevya.
"Mazingira ya kazi yamekuwa hatari sana kwa machifu katika eneo la Pwani. Wamekuwa wakivamiwa kila kuchao wanapokuwa wakitoka kazini, wakiwa kazini na hata nyumbani kwao,” alisema Shakilla.
"Wapewe bunduki angalau waweze kuwa na imani na kazi yao na kuichangamkia. Wengine huyashuhudia maovu yakifanywa lakini hawawezi hata chukua hatua kwa ukosefu wa silaha,” aliongeza mwakilishi huyo wa wanawake.
Shakilla aidha alisema kuwa hatua ya machifu na viongozi wa Nyumba Kumi kuuawa inashiria kwamba usalama ya mwananchi wa kawaida uko mashakani.
Mwakilishi huyo ametoa changamoto kwa serikali kushughulikia swala hilo kwa haraka.