Serikali imehimizwa kuzindua mpango wa kuwasajili wanafunzi kwa njia ya kielektroniki katika vyuo vikuu ili kubaini wanaotoweka vyuoni humo katika hali ya kutatanisha.
Kulingana na shirika la kielimu la ‘Undugu Mentorship Initiative’ Pwani, hiyo ndio njia pekee ya kuwatambua wanafunzi wanaohudhuria masomo na wale wanaotoweka vyuoni bila ya wahadhiri na wasimamizi wa chuo kutambua waliko.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Katibu wa Shirika hilo linalowaelekeza wanafunzi masomoni Reuben Shumma amesema kwamba hali inavyovikumba vyuo vikuu kwa sasa ni ya kutatanisha mno na ni lazima serikali iidhinishe mbinu hiyo ya kuwasajili Wanafunzi kupitia kwa njia ya kielektroniki.
"Tunapendekeza serikali kuzindua mpango wa kusajili wanafunzi kwa jia ya kielektroniki ili kuhakikisha kuwa inatambua wanafunzi kwa njia ya urahisi na kuzuia wanafunzi kutoroka madarasani wakati wa masomo," alisema Shumma.
Mdau huyo katika sekta ya elimu ameutaja mpango huo kama utakaowaondolea dhiki Wazazi katika eneo hili la Pwani hasa ikizingatiwa kwamba eneo hili limeshuhudia visa vingi vya Watoto kutoroka shuleni na kuhudhuria hafla za kujivinjari.