Waziri wa Kilimo Willy Bett amesema kuwa serikali inapania kuweka mikakati kabambe ya kukabiliana na visa vya ulaghai na utovu wa usalama katika Bahari Hindi.
Bett alisema kuwa kuna haja ya kuvikabili visa hivyo ambavyo vimeripotiwa kuongezeka katika siku za hivi majuzi, ili kuleta hali ya utulivu na kurejesha usalama katika maeneo hayo.
Akizungumza na wanahabari katika hafla ya ufunguzi rasmi wa kongamano la wadau mbali mbali katika sekta ya uvuvi na maswala ya ubaharia nchini, Bett alisema kwamba serikali kupitia wadau hao itajadili mbinu mwafaka zitakazotumika katika kudhibiti maovu yanayotekelezwa na wakiukaji wa sheria.
“Ni muhimu kuweka mikakati ambayo itaweza kusitisha au kupunguza visa hivi vya utovu wa usalama, kwa kuwa bahari imekuwa ikitumika vibaya na baadhi ya watu kwa ulanguzi wa binadamu na madawa ya kulevya na hata silaha,” alisema Bett.
Aidha, waziri huyo ametoa wito kwa wakaazi wanaoishi katika fukwe za bahari haswa wanaojihusisha na maswala ya uvuvi, kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa kwa idara za usalama wanapokumbana na matukio au shughuli wanazozishuku, ili kusaidia katika kuimarisha sheria na usalama.