Share news tips with us here at Hivisasa

Aliyekuwa mbunge wa eneo bunge la Nyaribari Chache, Chris Bichage, ameomba serikali ya kitaifa na ile ya Kaunti ya Kisii kuweka mikakati kabambe ya kuhakikisha watu ambao wanaishi sehemu zilizo chini na kwenye miteremko hawataathirika wakati wa mvua ya El Nino ambayo inatarajiwa kuanza kunyesha wakati wowote sasa.

Kulingana naye, watu ambao huishi katika sehemu mbalimbali kama vile Kiogoro, Nyanguru na sehemu zingine huathirika na kupata hasara mvua kubwa inaponyesha, jambo ambalo alisema halipaswi kushuhudiwa tena.

Akizungumza na waandishi wa habari Siku ya Alhamisi mjini Kisii, mwanasiasa huyo alisema serikali sharti ihakikishe hakuna mwananchi anaathirika kufuatia mvua hiyo inayotarajiwa kunyesha.

Bichage aliomba wakazi wa kaunti ya Kisii haswa wale wanaoishi katika sehemu zilizo chini na kwenye miteremko kuchimba mitaro ili mvua inapoanza, wasije wakaathirika pakubwa.

“Tunapotarajia mvua ya El Nino kuanza kunyesha, naomba kila mtu aweze kuwa makini kwani kuna sehemu ambazo huwa za kuhatarisha sana hapa Kisii,” alisema Bichage.

Aliongeza ”Wale ambao huishi sehemu zilizo chini na kwenye miteremko wahakikishe wamechimba mitaro ya kutosha na serikali iwasaidie ili wasiathirike.”

Wakati huo huo, mwanasiasa huyo aliomba wahudumu wa magari na waendeshaji bodaboda kutoendesha pikipiki zao kwa kasi wakati wa mvua na kuwa macho ili kulinda maisha ya watu.