Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wananchi katika Kaunti ya Mombasa wameitaka serikali na upinzani kutonyosheana vidole bali kufanya kazi pamoja ili kuboresha maisha ya mwananchi wa kawaida.

Wananchi hao wamesema kuwa ni jukumu la kila kiongozi kuwajibika katika kuimarisha maendeleo kwa taifa hilo, na kuwataka wanasiasa hao kukoma kushambuliana kwa misingi ya kisiasa isiyokuwa na umuhimu wowote.

Wananchi hao,  wakiongozwa na Halima Namai walisistiza siku ya Alhamisi walipohojiwa na mwanahabari huyu kuwa lazima uchumi wa nchi uimarike ili kila mwananchi aweze kujimudu kimaisha, hasa bei ya bidhaa muhimu kama unga, maziwa, mkate na mafuta ambazo bei yake zilipanda mwaka huu.

Wakazi hao pia wameitaka serikali kutekeleza manifesto yao kama walivyoahidi wakati wa uchaguzi ikizingatiwa kuwa ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana bado unashuhudiwa, matatizo ya ardhi zikiwemo nyinginezo.

Vilevile wamesema kuwa wakati huu ambapo tunaanza mwaka wa 2016, wana matumaini makubwa na baraza la mawaziri lililoteuliwa na rais ikizingatiwa kuwa rais alivunjulia baraza la hapo nyuma baada ya baadhi ya mawaziri kuhusishwa na ufisadi.

Aidha, wameitaka serikali kuwajibika pakubwa katika kupiga vita ufisadi kama njia moja wapo ya kuimarisha uchumi wa taifa hili.