Gavana wa jimbo la Nakuru Kinuthia Mbugua ameuliza idara za usalama wilayani Kuresoi kufanya kazi kwa pamoja ili kumarisha kero la wizi wa mifugo katika eneo hilo.
Wenyeji wa maeneo ya Sirikwa, Nyakinyua na Tayari wilayani humo walielezea gavana Mbugua jinsi ambavyo wanavyokesha nje usiku kucha kwa hofu ya kushambuliwa na wezi wa Ng’ombe.
“Bw.Gavana, usiku unapofika sisi badala ya kulala kwa amani kama wakenya wengine, jukumu letu ni kushika doria katika boma zetu tayari kupambana na wezi wa ng’ombe ambao hutuvamia nyakati za usiku. Hili limekuwa tatizo sugu ambalo linawakereketa wazee wa eneo hili,” alisema Kelvin Mburu.
Wakaazi hao wameuliza maafisa wa usalama, haswa wale wa kukabiliana na wezi wa mifugo kutumwa ili kushika doria katika maeneo mbali mbali wilayani Kuresoi, ambapo visa hivyo vimefikia viwango vya kuogofya.
“Tungependa kuuliza serikali, hizi ng’ombe ambazo huibwa kila siku hufichwa wapi. Kwa sababu tunaungana kama wakaazi na kufuata nyayo lakini hakuna ng’ombe ambao hupatikana,” alitaja mwenyeji mwingine.
Wananchi hao wamesema huenda wizi wa mifugo ukavuruga uwepo wa amani wakisema ni sharti serikali ikabiliane na wahuni wanaotekeleza uovu huo.
Gavana Mbugua kwa upande wake ameuliza wakaazi wilayani Kuresoi kujiepusha na uvujaji sharia, na badala yake kuishi kwa amani.
Aidha, ameuliza wananchi wa eneo hilo kushirikiana na kutoa riporti kwa maafisa wa usalama ili kukabiliana na wezi wa mifugo.
“Wale wanavamia boma za watu na kutoa mifugo zizini lazima wawe wanaishi miongoni mwenu. Nitaeleza kamshina wa kaunti tatizo lenu ili suruhu la kudumu lipatikane,” alitamka Gavana.