Chama cha walimu wakuu wa shule za upili katika wilaya ya Kisii ya kati kaunti ya Kisii wameomba serikali kuu kuongeza pesa kwa shule haswa kwa mradi wa masomo ya bure kwani zile wanazotoa hazitoshi.
Akiongea na wanahabari siku ya Jumatano katika mji wa Kisii, mwenyekiti wa chama hicho Timothy Atuti alisema kila mwanafunzi akipokezwa shillingi 2,000 kwa muhula wa pili hazitatosha kwa kuendeleza masomo.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa wanafunzi wanastahili kupokezwa 50% katika muhula wa kwanza, 30% muhula wa pili na 20% katika muhula wa tatu pesa ambazo amesema huchelewa kufika katika mashule.
Aliomba serikali ihakikishe kuwa pesa hizo hufika shuleni wakati unaofaa.
“Pesa ambazo hutumwa kwa shule huchelewa sana. Tunaomba serikali kuzituma pesa hizo mapema na ziwe zimeongezwa kidogo ili elimu iweze kunawiri kwa kiwango kile kinachostahili,” alisema Atuti.
Wakati huo huo, chama hicho kilisema ili elimu kuinuka zaidi katika mashule mbalimbali humu nchini, sharti pesa ziwe zinafika kwa shule mapema ili ziwe zinafanya yale yanastahili kufanywa mapema kama njia moja ya kuzuia wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa.
Walisema ni jukumu la serikali kuu kuangalia suala hilo kwa kina na kulishughulikia vilivyo.