Wasimamizi wa taasisi ya Enchoro, iliyoko wadi ya Gesima, kaunti ya Nyamira wameiomba serikali kuu kuwaajiri walimu katika taasisi hiyo.
Akiongea siku ya Alhamisi katika taasisi hiyo wakati wanafunzi walifungua kwa kipindi cha pili, mwenyekiti wa taasisi hiyo Peter Minyira aliiomba serikali kuu kuwaajiri walimu katika taasisi hiyo kwa kuwa hawana walimu wa kutosha.
“Ninaomba serikali kuu kuwaajiri walimu ili tuweze kupata walimu wa kutosha watakaofunza wanafunzi hawa, kwa sasa walimu ni wachache na wanafanya kazi ngumu kwa kufunza somo zaidi la moja kwa sababu ya ukosefu wa walimu hao,” alihoji Minyira.
Kulingana na Minyira, walimu wakiongezwa katika taasisi hiyo wanafunzi watapata mafunzo katika mazingira mazuri.
Aidha, taasisi hiyo, kupitia kwa mwenyekiti huyo wamepongeza Serikali ya Kaunti ya Nyamira kwa kujenga darasa moja ambalo kwa sasa ni msaada kubwa kwao.
“Tunaipongeza Serikali ya Kaunti ya Nyamira kwa kutukumbuka na kujenga darasa moja ambalo watoto wetu wanatumia kwa sasa,” alisema Bosire Evans, mzazi.
Wazazi wengine wa Taasisi hiyo wameipongeza serikali kuu kwa kuleta mpango wa kula shuleni ambao umesaidia wanao.
Aidha, wanafunzi katika taasisi hiyo, ambao wengi hutoka mbali, wameiomba serikali ya kaunti kuwajenjea bweni ili kuwasaidia kutosafiri mda mrefu kufika taasisini humo.
“Tunaomba serikali ya kaunti kutujengea bweni kwa kuwa wanafunzi wengi hutoka mbali na wengi wao huchelewa shuleni, lakini tukijengewa tutafaidika pakubwa,” alihoji Minyira.
Kwa wakati huo huo, amewaomba wanafunzi kujiunga na taasisi hiyo ili kujiendeleza na masomo.