Takriban maskwota elfu 10 katika Shamba la Vipingo kaunti ya Kilifi wameapa kukaidi amri ya kuhama katika shamba hilo la hekari elfu 11 wakidai kuwa ardhi hiyo ni yao tangu jadi.
Wakaazi hao wamesema kuwa bwenyenye mmoja mmiliki wa kampuni ya Centum limited anashirikiana na baadhi ya watu fulani kuwafurusha kwa ardhi hiyo licha ya kuwa wakaazi hao walikubaliana katika makataba waliyosaini na miliki halali wa ardhi hiyo mwenye kampuni ya vipingo Estate.
Wakaazi hao waitaka serikali kuu, tume ya kitaifa ya ardhi nchini na ule ya kaunti ya Kilifi kuingilia kati mzozo huo na kuwasaidia wakaazi hao wanaodai kuwa ardhi hiyo ni yao na wala hawana pakwenda.
Naye Seneta wa kaunti ya Kilifi Stewart Mwadzayo ameitaka serikali ya Jubilee kuingilia kati na kuhakikisha kuwa wakaazi hao wanasalia katika ardhi hiyo ili kuzuia kushughudiwa kwa mgogoro wa ardhi ambayo huenda ukasababisha hata maafa.
"Tunaitaka serikali kuu kuingia kati swala hili na pia tume ya kitaifa ya ardhi ili kuhakikisha kuwa haki za wakaazi hawa wa vipingi inapatika kwa sababu iwapo watafurushwa basi wataenda wapi ila mgogoro ndio tunahofia kushughudiwa na sisi kama viongozi tunapenda watu waishi na amani," alisema Madzayo siku ya Jumanne katika eneo la Vipingo.
Migogoro ya ardhi katika ukanda wa Pwani inazidi kushughudiwa kufuatia kwa kukithiri kwa unyakuzi wa ardhi kila uchao na kusababisha wakaazi wengi kusalia maskwota licha ya kuwa wamiliki halali wa ardhi hizo.