Mwenyekiti wa wakimbizi wa ndani walioathirika kufuatia ghasia zilizozuka baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 katika katika kaunti za Nyamira na Kisii ameomba serikali kuu kuwachukulia hatua kali ya kisheria wale wanajitambulisha kuwa wakimbizi ili kufadhiliwa na serikali.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea siku ya Jumatano na waandishi wa habari katika uwanja wa michezo wa Gusii, mwenyekiti huyo Nemuel Momanyi alisema kuna baadhi ya watu ambao wanajitambulisha kuwa wakimbizi wa ndani ilhali hawakufurushwa kutoka popote ila ni mbinu ya kufadhiliwa na serikali ya kitaifa.

Hii ni baada ya wakimbizi wa ndani 23,000 katika eneo la Gusii wanaostahili kufadhiliwa na serikali kusema kuwa hawajawahi pata msaada wowote kutoka kwa serikali hadi sasa.

“Kuna watu ambao wanasema ni wakimbizi wa ndani hapa Kisii. Wakimbizi hao bandia walifadhiliwa na serikali na wakimbizi wa ndani halisi hawakupata chochote. Naomba serikali iwachukulie hatua kali ya kisheria,” alisema mwenyekiti wa waathiriwa eneo la kisii.

“Si vizuri watu kupata pesa za waathiriwa huku wakisema hao ni waathiriwa. Tunahitaji haki itendeke kwa wananchi wote kote nchini,” aliongezea Momanyi.

Wakati huo huo mwenyekiti huyo alisema kuwa ni wakimbizi hao bandia wanaishi vizuri baada ya kupata pesa za bure kutoka kwa serikali ilihali wale halisi wananasumbuka.

“Tunaomba serikali itukumbuke kama ilivyokumbuka waathiriwa wengine katika sehemu zingine hapa chini,”alisema Momanyi.