Serikali kuu pamoja na ile ya kaunti zimeombwa kujitahidi kuhakikisha kuwa hospitali kuu ya ukanda wa Pwani, Coast General, inapata mashine maalum ya kukagua na kutibu saratani.
Mashine hiyo inayofahamika kama 'Radiotherapy Machine' inadaiwa kuwa moja tu hapa nchini, huku wagonjwa wengi wakishindwa kupata huduma hizo kutokana na gharama kuwa juu.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumanne mjini humo, Erick Amisi muuguzi katika kituo kinachoshughulikia watu wanaougua magonjwa sugu cha Coast Hospice, alisema kuwa mara nyingi hulazimika kuwatuma wagonjwa mjini Nairobi.
“Huduma za hii mashine ni ghali mno kwa sababu inapatikana mjini Nairobi peke yake. Mara nyingi tukiwatuma wagonjwa wetu huko, wanashindwa kwenda kutokana na gharama ya juu ya usafiri na matibabu pia,” alisema Amisi.
Hospitali kuu ya mkoa wa pwani haina mashine hiyo, hali iliyosabaisha changamoto kubwa kwa wakaazi wa maeneo hayo kwani ndio hospitali ya kipekee inayotegemewa zaidi na wakaazi.
“Ningeomba serikali ya kaunti kama vile inavyojitahidi kupata ufadhili wa miradi mbalimbali pia itafute ufadhili wa kupata hii mashine ili tujaribu kupunguza gharama ya matibabu,” alisema Amisi.
Kulingana na madaktari ni kuwa zoezi la kupata matibabu ya saratani kupitia mashine hiyo ni ghali mno ambapo mgonjwa mmoja hutakiwa kulipa takriban shilingi elfu 10 kila anapozuru hospitali kwa matibabu.
Utafiti kutoka katika kituo hicho cha Coast Hospice unaonyesha kuwa idadi kubwa ya watu wanaougua saratani ni wanawake ambapo wengi wao husumbuliwa na saratani ya matiti pamoja na ile ya kizazi.
Iwapo mpango wa kuweka mashine ya Radiotherapy katika hospitali ya mkoa wa Pwani itafaulu, basi gharama ya matibabu itapungua huku idadi ya vifo vinavyotokana na saratani vikitarajiwa kupungua