Siku kuu ya uhamasisho kuhusiana na ulemavu wa ngozi maarufu kama ‘World Albinos Awareness Day’ ilikamilika siku ya Jumamosi.
Mmoja wa wakaazi wa mji wa Kisii ambaye ni zeruzeru amewashtumu vikali wasimamizi wa mashirika yanayoangalia maslahi yao.
Fred Omwoyo Ong’era ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Mount Kenya, akisomea shahada ya taaluma ya elimu mwaka wa nne, alielezea maskitiko yake kufuatia baadhi ya viongozi wao kukosa kuonyesha uongozi bora wanaposhughulikia masuala mengi yanayowasonga.
Alidokeza kuwa baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakifuja hela ambazo zinalenga kuwafadhili zeruzeru kujiendeleza kielimu.
“Pesa nyingi zinazokuja kutoka kwenye mashirika mbali mbali pamoja na serikali haziwafikii walengwa kwa sababu ya ulafi na ufisadi miongoni mwa viongozi na wasimamizi. Naiomba serikali iangazia masuala yetu ili kuhakikisha kuwa kuna uwazi kwenye matumizi ya pesa,” alisema Omwoye.
Hata hivyo, alionyesha matumaini yake kuwa kutatokea mabadiliko ikiwa wataendelea na makongamano kama haya ya kila mwaka, ya kujadili masuala mbali mbali yanayowalenga.
Kumeshuhudiwa malalamiko kutoka kaunti ya Kisii kuhusiana na jinsi mashirika ya watu wenye ulemavu yanaendeshwa.
Jambo hilo limesababisha baadhi ya wanachama wa makundi hayo kujiuzulu.