Serikali ya kitaifa imeongeza kiwango cha pesa ambazo mayatima, walemavu, wajane na waliozeeka hufadhiliwa kutoka shillingi millioni 200 hadi billioni 18.7 kila mwaka.

Share news tips with us here at Hivisasa

Hii ni baada ya idadi ya watu kuendelea kuongezeka nchini kila uchao huku ikibainika kuwa wale ambao tayari wamesajiliwa kupata usaidizi huo ni watu 770,000 kote nchini.

Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Omobera eneo bunge la Bomachoge Borabu afisa wa wafanyikazi wa serikali Susan Mochache alisema serikali iliongeza pesa hizo ili watu hao wapate usaidizi katika kujikimu kimaisha.

Afisa huyo alisema serikali inalenga kusajili watu millioni moja huku akisema shughuli ya kusajili wengine inaendelea ili watu wa aina hiyo wapate usaidizi.

“Serikali imeongeza pesa za ufadhili na ninaomba yeyote anayepata pesa hizo azitumie vyema kukabili umaskini na kujiendeleza kimaisha ,” alisema Mochache.