Serikali imeombwa kubadilisha nia yake ya kumpokonya Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho, bunduki.
Kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Jumanne, Mwenyekiti wa Supkem Kaunti ya Kilifi, Sheikh Salim Dima, alisema hata ikiwa serikali ina nia njema, imefanya uamuzi huo wakati ambao sio mwafaka.
Dima alisema kuwa hatua hiyo huenda ikatafsiriwa kuwa ni ulipizaji wa kisasi kwa chama kinachotawala kushindwa katika uchaguzi mdogo wa Malindi.
Aidha, alisisitiza kuwa serikali inafaa kuwaambia Wakenya ni makosa gani Gavana Joho alifanya kupitia silaha alizonazo.
Hatua hiyo ya kumataka Gavana Joho kurejesha bunduki zake imejiri siku chache tu baada ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Malindi, huku ikidaiwa kuwa viongozi wa mrengo wa Cord walitumia mamlaka yao vibaya kuwashurutisha walinzi wao kuwanyanyasa wakaazi.
Waziri wa maswala ya ndani nchini Meja Jenerali mstaafu Joseph Nkaissery alisema Gavana Joho anaweza kukata rufaa kuhusiana na uamuzi huo ikiwa kwanza atarejesha bunduki alizopewa na serikali kutumia kama ulinzi wake.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Nkaissery alisema kuwa Joho amekuwa akionekana mwenye hasira na hali yake inaweza kumfanya atumie bunduki yake visivyo.
Nkaissery alishikilia msimamo wake kuwa Gavana Joho lazima asalimisha bunduki zake zote anazomiliki kwa maafisa wa polisi, na kuongeza kuwa endapo atazidi kukaidi agizo hilo, atatiwa mbaroni.