Abiria katika kivuko cha feri cha Likoni hapo awali. Picha/ barakafm.org
Shinikizo zinazidi kutolewa kwa serikali kuliwajibikia kwa haraka swala la kukizindua upya kivuko cha feri cha Mtongwe.
Joseph Mositet, ambaye ametangaza azma yake ya kuwania kiti cha wadi ya Mtongwe, alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona msongamano wa mara kwa mara ukishuhudiwa katika kivuko cha Likoni.Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Mositet aliitaka serikali kulipa kipau mbele swala hilo ili kupunguza msongamano katika kivuko cha Likoni.Mwanasiasa huyo alisema kwamba ukosefu wa kivuko katika eneo la Mtongwe umechangia kushuhudiwa kwa idadi ndogo ya watalii wanaozuru sehemu za kusini mwa Pwani, kwani wanaogopa msongamano katika kivuko cha Likoni.Mositet aidha amedokeza kwamba endapo swala hili litapigiwa upato, basi viwango vya uchumi katika ukanda wa Pwani na kote nchini kwa jumla vitaimarika.