Shirika linalosimamia rasilmali kwenya kaunti ya Kwale kwa ushirikiano na kampuni ya Bamburi Cement limetangaza kuwa litapanda miti takriban milioni tatu kama njia moja wapo ya kudumisha mazingira bora.
Akiongea na mwanahabari baada ya mkutano wa kimazingira mjini Mombasa siku ya Ijumaa, mshirikishi wa shirika linalosimamia misitu kaunti ya Kwale Mohamed Ali, ameeleza kuwa huenda vizazi vijavyo vikakosa mazingira bora iwapo jamii itaendelea kuaharibu mazingira kwa kutaka miti kiholela.
Mohamed ametaka kuwepo kwa sheria maalum itakayolinda ukataji wa miti kwani tabia hiyo imekuwa ikiendelea hata kwa misitu ya Kaya ambayo mingi ya misitu sasa imenyakuliwa na mabwenyenye na kuwa ardhi binafsi za kuekeza.
“Tunaiomba serikali kuibuka na sheria kali zaidi dhidi ya wanataka miti na kuharibu mazingira kwani hatua hii husababisha ukame kutokana na kukosekana kwa miti ya kuvutia mvua," alisema Mohammed.
Swala hilo limeungwa mkono na Mwenyekiti wa Wazee wa Kaya Abdallah Mnyenze aliyeitaka serikali kuwachukulia hatua wanaokata miti kiholela kwa kigezo cha umaskini jambo linalosababisha kupanda kwa bei ya bidhaa kila uchao.
Hatua hii inajiri baada ya kuonekana wengi wa wakaazi wakikata miti kiholela hususan mti wa Mnazi na kufanya mbao za kujengea makaazi yao.