Mkereketwa na mtetezi wa haki za kibinadamu katika kaunti ya Nakuru David Kuria ametoa wito kwa serekali ya kaunti hiyo kutafuta suluhu la kuwasaidia watoto wanaorandaranda mitaani.
Akiongea na mwandishi wetu Jumamosi hii, mwanaharakati huyo ambaye anasimamia shirika kwa jina la Nahurinet (Nakuru Human Rights Network) amesema kuwa serekali ya kaunti iko na wajibu wa kuwapeleka watoto hao wa mitaani katika vituo vya kurekebisha tabia na baadaye kuwapeleka shule.
Amesema kuwa wengi wa watoto hao ambao wamejaa mjini Nakuru na katika miji mingine huishia kuwa majambazi na kuwahangaisha wananchi.
Ameongeza kuwa vijana hao huanza wizi wa mikoba ya wanawake na pia kuingia mifuko ya watu haswaa wale wanaosafiri kutoka eneo moja hadi jingine.
Halkadhalika, amesema kuwa watoto wanarandaranda mitaani wengi wao wamekuja mjini Nakuru kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/2008, na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe katika baadhi ya jamii za humu nchini.
Haya yanajiri wakati kumeeshuhudiwa idadi kubwa ya watoto hao katika miji mingi kote nchini.