Huku mamia ya maelfu ya Waislamu wakikongamana katika miskiti na viwanja mbali mbali kwa swala ya Eid ul fitri siku ya Alhamisi, serikali ya Kenya imetakiwa kutizama upya mahusiano yake na serikali ya Israel.
Serikali ya Kenya chini ya uangalizi wa Rais Uhuru Kenyatta imeombwa kuusitisha mara moja uhusiano huo wa kitaifa, kijasusi na kibiashara kwa manufaa ya Wakenya wote wapenda amani.
Wito huo umetolewa na aliyekuwa kadhi mkuu wa Kenya Sheikh Hamad Kassim, baada ya kuongoza waumini kwenye swala ya Eid.
Sheikh Hamad ameitanabaisha serikali kuwa miongoni mwa mikataba ya kijasusi ambayo Kenya imeweka na taifa la Israel kupitia waziri wake mkuu Benjamin Netanyahu, huenda ikalitumbukiza taifa katika mashambulizi zaidi ya kigaidi kinyume na matarajio ya Wakenya wengi.
Taifa la Israel linatuhumiwa kuikalia kwa mabavu Palestina huku umoja wa mataifa ukishtumiwa kwa kulinyamazia suala hilo.
Ziara ya Netanyahu humu chini imepokea pingamizi kutoka kwa baadhi ya viongozi haswa wa dini ya Kiislamu.