Mkurugenzi mkuu wa shirika la Sauti ya Wanawake ameitaka serikali kutenga fedha zaidi ili kufanikisha vita dhidi ya dhuluma za kijinsia humu nchini.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa, Bi Violet Muthinga alisema sharti serikali itenge fedha za kutosha katika hamasa na vita dhidi ya dhuluma za kijinsia kwa kuwa familia nyingi katika ukanda wa Pwani zimeathirika na swala hilo.

Bi Muthinga alisema visa vya akina mama na watoto kudhulumiwa vimeongezeka mara dufu, na ni jukumu la serikali pamoja na wadau wanaohusika na swala hilo kulijadili kwa kina, ili kuweka mikakati na mbinu zitakazosaidia katika kulikabili.

“Hospitali na zahanati katika eneo la Pwani kamwe hazina vitengo maalum vya kuwashughulikia waathiriwa wa dhuluma za kijinsia hali ambayo imewanyima haki wahasiriwa hao,” alisema Bi Muthinga.

Vile vile, afisa huyo wa kupambana na dhuluma za kijinsia amesisitiza umuhimu wa vituo vyote vya polisi katika eneo la Pwani kuwa na eneo maalum na maafisa walio na ufahamu kuhusiana na maswala ya dhuluma za kijinsia, ili kuwahudumia waathiriwa vyema.