Viongozi mbalimbali katika sekta ya elimu pamoja na wale wa kidini katika eneo la Pwani wametoa wito kwa serikali za kaunti kushirikiana na serikali kuu kutoa vifaa zaidi vya kusomea kwa wanafunzi wanaoishi na ulemavu.
Akizungumza katika eneo la Kaloleni, Afisa wa elimu katika Kaunti ndogo ya Rabai Sebastian Muzungu, alisema kuwa Wizara ya Elimu bado ina mengi ya kutimiza kwa wanafunzi hao, kwani idadi ya shule za watoto wanaoishi na ulemevu ni kidogo ikilinganishwa na wale wanaojiunga na shule hizo.
Muzungu alisema kuwa vifaa vya kutoa huduma za masoma kwa wanafunzi hao vinaendelea kupungua kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi walemavu, huku akiongeza kuwa hatua hiyo itakuwa mojawapo ya mbinu za kuinua viwango vya elimu katika eneo la Pwani pasi ubaguzi wa ulemavu.
Afisa huyo alisisitiza kuwa ipo haja ya serikali za kaunti kupitia Wizara ya Elimu kubuni mbinu mpya za kujenga madarasa zaidi yaliyo na vifaa vya kutosha katika kila kaunti Pwani ili watoto wanaoishi na ulemavu wapate nafasi ya kufurahia haki yao kupata elimu bora.
Mchungaji Fred Mangi wa kanisa la Gospel Ministries, alisema kuwa mradi walioanzisha katika Shule ya msingi ya Kizurini umeendelea kuwasaidia wanafunzi wengi ila kwa sasa madarasa na vifaa vya shule hiyo vinazidi kuwa finyu kutokana na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na shule hiyo.
Alisema serikali inapaswa kubuni mbinu mbadala ya kuhakikisha kuwa wanaoishi na ulemavu wanajengewa shule zenye mabweni na kuandikiwa walimu wa kutosha ili kuwapa motisha wa kuzingatia umuhimu wa masomo kama nguzo kuu maishani.
Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Mbunge wa Kaloleni Gunga Mwinga ambaye alisema kuwa wanaoishi na ulemavu pia wanauwezo wa kuzingatia masomo na kuwa wenye manufaa katika jamii.