Mkuu wa Idara ya Kilimo Kaunti ya Mombasa Anthony Njaramba ameitaka serikali kulipa fidia za wakaazi na wavuvi waliopoteza makaazi yao kutokana na kutoa nafasi kwa ujenzi wa reli ya SGR.
Akizungumza katika hafla ya kuzindua rasmi boti la uvuvi MV Mombasa 001 jijini Mombasa, Njaramba alisema kuwa mradi huo wa SGR umekosesha familia nyingi amani kwani waathiriwa waliokua wakitegemea uvuvi wameshindwa kujikimu kimaisha.
Njaramba alieleza kuwa zaidi ya wavuvi 1700 wameathirika na ujenzi huo na wamekuwa wakisubiri fidia ambayo hawajapokea hadi leo.
Alielezea kutamaushwa na hatua ya serikali kufidia waathiriwa katika maeneo mengine nchini na kutowashughulikia walioko katika ukanda wa Pwani.
“Hii sio haki kabisa kwani serikali inajua wavuvi hawa wamekuwa wakitegemea bahari kama kitega uchumi chao cha kila siku,” alisema Njaramba.
Aidha, alisema kuwa kucheleweshwa kwa kulipa fidia hizo kumewanyima wavuvi na wakaazi wa maeneo athirika mtaji walioazimia kuanzisha nao biashara ili kujiendeleza kimaisha.
Baadhi ya maeneo yaliyoathirika ni Mkupe, Sunza, Changamwe na viunga vyake.