Serikali imetakiwa kuwapa wakaazi wa taarafa ya Olenguruone wilayani Kuresoi hatimiliki za ardhi, huku wenyeji wakisema ukosefu wa hati miliki unachangia ongezeko la mizozo ya mashamba.
Wakazi hao wanaojumuisha maskwota waliopewa makao na chini ya serikali za Rais wastaafu Daniel Arap Moi na Mwai Kibaki baada ya kufurushwa kutoka msitu wa Mau, wamesema bado hawajapata hatimiliki za mashamba yao kutoka kwa wizara ya ardhi licha ya kutimiza masharti yote.
Diwani wa zamani wa Tinet Bw David Sitienei Alhamisi alisema baadhi ya wenyeji wamepokonywa mashamba yao na watu mashuhuri ambao hushirikiana na maafisa fisadi serikalini kulaghai wale ambao hawana hatimiliki.
Sitienei amemtaka waziri wa ardhi Joseph Kaimenyi pamoja na mwenyekiti wa tume ya ardhi nchini NLC kuzuru eneo hilo na kuanzisha harakati za kuwapa wakaazi stakabadhi hizo za umiliki wa ardhi kama inavyofanyika katika maeneo mengine nchini.
“Imekuwa ni vigumu kwa wakaazi hawa kujiendeleza kiuchumi kwa sababu hawana hati miliki za mashamba yao. Kupata mikopo kwenye benki pia ni tatizo japo hofu kubwa ni mashamba yao kunyakuliwa na wanasiasa,” alisema Sitienei.
Alisema serikali itaweza kulinda chemchemi za maji iwapo itawapa wananchi stakabadhi hizo pamoja na kutambua ardhi za umma.