Viongozi mbali mbali katika kaunti ya Nakuru wameitaka serikali kuu kufadhili serikali za kaunti ili kugharamia vyombo vya kisasa vya matibabu katika hospitali za umma.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakiongozwa na gavana Kinuthia Mbugua, viongozi hao wamesema ingawa huduma za afya zimegatuliwa kutoka serikali kuu hadi zile za  kaunti, baadhi ya vyombo vya kutoa matibabu ni ghali mno na huenda serikali za kaunti zikakosa fedha ili kununua zana za matibabu kwa hospitali na zahanati zote za umma katika jimbo.

Gavana huyo amesema wananchi wanaohitaji matibabu maalum hulazimika kutibiwa nje ya nchi kwa gharama kubwa, huku akiitaka serikali kuhakikisha kuna wataalam wa kiafya wa kutibu magonjwa sugu kama vila saratani.

Kauli yake imeungwa mkono na mbunge wa Molo, Jacob Macharia, ambaye ameuliza wananchi kujisajili kwa mpango wa huduma ya bima ya afya NHIF, ili kuepuka changamoto za kulipa bili ya hospitali.

Mbunge huyo amesema baada ya serikali kuzindua huduma ya kujifungua bila malipo katika hospitali zote za umma, idadi ya watoto ambao hufaliki baada ya kuzaliwa imepungua.

Mwakilishi wa wadi ya Turi Michael Wang’ombe, Ngugi Muigai (Molo) na mwakilishi maalum Beatrice Nyawira wamesema ni sharti wananchi wahamasishwe na idara ya afya jinsi ya kukabiliana na magonjwa ambukizi.

Wamesema mtindo wa kina mama kujifungua watoto bila kwenda hospitalini umepungua, wakisema hatua hiyo imeafikiwa baada ya serikali na mashirika mengine kuwa kwenye mstari wa mbele kuwahamasisha umma umuhimu wa kutafuta tiba hospitalini kinyume na awali ambapo wananchi wangetumia dawa za kienyeji.