Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu wa Rais William Ruto amesema kuwa serikali imetenga zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ujenzi wa vyuo vya kiufundi katika Kaunti ya Mombasa.

Ruto alisema kuwa vyuo hivyo vitajengwa katika eneo la Likoni na Changamwe, huku mradi huo ukilenga sana vijana wanaotoka katika sehemu hizo.

Akizungumza huko Likoni siku ya Jumamosi, Ruto alisema kuwa kupitia kwa vyuo hivyo, vijana watapata fursa ya kujifunza ujuzi wa aina mbalimbali ili kusaidia katika maendeleo ya taifa.

“Tumeshakubaliana na mbunge wa Likoni pamoja na mtukufu rais kwamba tutajenga vyuo hivyo hapa ili vijana wetu wanufaike na kuondoa tatizo la ukosefu wa kazi,” alisema Ruto.

Takwimu zinaonyesha kwamba eneo la Likoni limezoroteka sana kielimu, huku watoto wengi wakiachia masomo yao katika shule ya msingi.

Wakati huo huo, Ruto amemtaka Gavana wa Mombasa Hassan Joho kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo kwenye eneo hilo na kukoma kutoa lawama kila wakati.

“Najua gavana umechaguliwa na watu wa Mombasa na tunakuheshimu sana. Nakuomba tushirikiane pamoja bila kutia siasa katika kila jambo angalau wanachi wetu wafaidike,” aliongeza Ruto.

Kauli ya naibu rais inatokana na matamshi aliyotoa Gavana Joho kwamba Rais Kenyatta amekuwa akimkwepa tangu azuru Mombasa kwa madai kwamba wanatoka katika mirengo tofauti ya kisiasa.