Serikali kuu imetangaza kutenga kima cha shilingi milioni 700 kuboresha Hospitali kuu ya ukanda wa Pwani, ili kufikia kiwango cha 'level five'.
Vile vile, serikali imetangaza kutenga kima cha shilingi milioni 400 kuboresha hali ya Hospitali ya Kaunti ndogo ya Likoni, kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya katika Kaunti nzima ya Mombasa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Naibu Rais William Ruto alisema kuwa Serikali kuu imechukua hatua hiyo ili kuona kwamba wakaazi wa Mombasa wanapata huduma bora za afya.
Ruto alisema kuwa japo sekta ya afya imegatuliwa, serikali kuu ingali na jukumu la kuhakikisha kuwa hadhi ya vifaa vya matibabu mashinani inaimarishwa, ili kila Mkenya apate tiba inayofaa karibu na maeneo anayoishi.
“Tumetenga shilingi milioni 700 kuboresha Hospitali kuu ya ukanda wa Pwani na shilingi milioni 400 katika Hospitali ya Kaunti ndogo ya Likoni,” alisema Ruto.