Serikali imetoa tahadhari kwa wakaazi wa Mombasa kuwa waangalifu zaidi dhidi ya mashambulizi ya kigaidi.
Msemaji wa serikali Eric Kiraithe, amewataka wakaazi kutoa ripoti iwapo watapata habari zozote kuhusu mashambulizi ya kigaidi.
“Ningependa kuwahimiza wakaazi kutoa ripoti kwa polisi ili hatua za haraka kuchukuliwa,” alisema Kiraithe.
Kiraithe aidha alisema kuwa kuna taarifa za kijasusi kuhusiana na shambulizi la kigaidi katika Kituo cha polisi cha Central, japo haziwezi kutolewa kwa sasa.
Aidha, alisema kuwa huenda magaidi wanapanga shambulizi kama hilo, kutokana na shambulizi hilo la kwanza kutibuka.
“Serikali imeanzisha uchunguzi kubaini iwapo wanachama wa kundi la kigaidi la Islamic State walihusika katika jaribio la shambulizi lililotekelezwa katika kituo cha polisi cha Central,” alisema Kiraithe.
Msemaji huyo wa serikali aliwahakikishia wakaazi kuwa usalama umeimarishwa zaidi katika vituo vya polisi nchini.
Kauli hii inajiri baada ya shambulizi la kigaidi katika kituo cha polisi cha Central jijini Mombasa, ambapo washukiwa watatu waliuawa.