Wanachama wa mrengo wa Cord kutoka Mkoa wa Pwani walipata afueni siku ya Alhamisi baada ya mahakama ya Malindi kuagiza idara ya usalama kutowatia nguvuni wala kuwahangaisha.
Katika uamuzi wake, Jaji Shendi Chitembi aliagiza idara ya usalama kutowakamata viongozi wa Cord wanaodaiwa kuhusika katika vurugu zilizoshuhudiwa katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi, hadi kesi waliowasilisha mahakamani isikizwe na kuamuliwa.
Katika kesi hiyo, mawakili watano wa Cord wakiongozwa na James Orengo, wamevitaka vyombo vya usalama kukoma kuwaandama na kuwatishia viongozi wa mrengo huo mara kwa mara.
Kesi hiyo ilihudhuriwa na vinara wa Cord Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Moses Wetengalua, Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho pamoja na wabunge wa mrengo huo kutoka Mkoa wa Pwani.
Siku ya Jumatatu wiki hii, Joho aliagizwa na wizara ya usalama wa ndani ya nchi kuandikisha taarifa na idara ya usalama kuhusiana na vurugu zilizoshuhudiwa katika uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Malindi mnamo Machi 7.
Haya yanajiri juma moja tu baada ya Joho kupokonywa walinzi wake huku jaribio la idara ya usalama kutaka kumpokonya bunduki anayomiliki ikikosa kufaulu baada ya kupewa kibali na mahakama.