Serikali za kaunti zimeombwa kusitisha ukopaji wa fedha kutoka kwenye mashirika mbalimbali yakifedha ili kuepusha visa wa ukosefu wa fedha kwenye kaunti hizo siku za usoni.
Akiongea siku ya Jumapili kwenye hafla yakuchangisha pesa kule Rigoma katika eneo bunge la Kitutu Masaba, mwaniaji wa ugavana kwenye kaunti hiyo Bw Charles Mochama alisema kuwa kaunti nyingi hushindwa kujimudu kutumia fedha wanazopata kutoka kwa ushuru.
"Kaunti nyingi hushindwa kujimudu kwa kutumia pesa wanazo kusanya kama ushuru na badala yakutafuta mbinu yakuimarisha mapato yao, kaunti hizo huonelea heri kukopa," alisema Mochama.
Mochama ambaye vilevile ni mshauri wa kifedha wa benki ya dunia tawi la Kenya, alisema kuwa ukopaji wa aina hiyo huenda ukasababisha serikali za kaunti kukosa fedha zakuendesha shughuli zao katika siku za usoni.
"Ukopoji wa fedha nyingi kutoka kwa mashirika ya kifedha huenda ukasababisha serikali za kaunti nyingi kukosa pesa zakuendesha shughuli zao kwa siku zijazo,” alisema Mochama.
Mochama vilevile aliongeza kwa kusema kuwa baadhi ya kaunti huwarai wawekezaji wa kigeni kuekeza kwenye kaunti zao kwa kukopa huku akiziomba serikali za kaunti kutafuta mbinu zakuzalisha pesa badala yakukopa kwa maana ukopaji wa aina hiyo huenda ukaathiri maendeleo.