Mkuu wa Idara ya Elimu katika Kaunti ya Kilifi Salma Ahmed amezitaka serikali za kaunti katika eneo la Pwani kushughulikia matatizo ya uhaba wa chakula shuleni kabla ya muhula wa pili kuanza mwezi Mei.
Akizungumza katika katika Shule ya msingi ya Mnarani huko Kilifi, Ahmed alisema kuwa ikiwa viongozi wanataka viwango vya elimu katika kaunti za Pwani viongezeke kwa kutoa wanafunzi bora, basi ni sharti Wizara za Elimu kuanza kushughulikia tatizo la uhaba wa chakula katika shule mbali mbali mashinani kwa kuwa tatatizo hilo huchangia pakubwa katika matokeo ya wanafunzi wa shule za msingi.
Ahmed alisema kuwa familia nyingi kutoka eneo la Pwani zinajitahidi kuhakikisha kuwa zinawapeleka wanawao shuleni ila watoto hao wanapofika shuleni, hukosa hata maji ya kunywa jamba ambalo amelitaja kama kuwaathiri pakubwa.
“Walimu wanaowafundisha watoto wa shule za msingi huwa na wakati mgumu kwa kuwa wanafunzi wengi huanza kulala darasani kutokana na njaa,” alisema Ahmed.
Hatahivyo, Ahmed alisema kuwa serikali za kaunti za Pwani zinajitahidi ili kutatua swala hilo na kuhakikisha kwamba wanafunzi wanasoma bila ya kutatizika, ili eneo la Pwani liweze kutoa wanafunzi bora katika mtihani wa kitaifa ya mwaka ujao.