Serikali za kaunti zimetakiwa kuunda hazina yao ya Uwezo ili kuwanufaisha vijana na kina mama ambao hawajanufaika na hazina kuu ya uwezo inayoendeshwa na serikali ya kitaifa.
Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri alisema kuwa pesa zilizotengewa hazina ya uwezo ni chache mno na haziwezi kutosheleza mahitaji ya maelfu ya makundi ya vijana na akina mama kote nchini.
Akiongea katika eneo bunge lake siku ya Jumapili alipowapokeza hundi za pesa za uwezo vijana na kina mama, Ngunjiri alisema kuwa itakuwa vyema iwapo serikali za kaunti zitazindua hazina yao ya uwezo ili kuyafikia makundi mengi zaidi.
“Serikali kuu imejitahidi katika kuimarisha maisha ya vijana na kina mama kupitia hazina ya uwezo, lakini pesa hizo ni kidogo sana na haziwezi kufikia makundi yote kote nchini na ndio maana nahimiza serikali zetu za kaunti kutenga pesa kiwango fulani ili makundi ya vijana na kina mama yanayokosa pesa za serikali kuu yaweze kunufaikapia kifedha,” alisema Ngunjiri.
Mbunge huyo pia alisema kuwa serikali za kaunti zinaweza kupunguza viwango vya umaskini katika kaunti kupitia hazina kama ya uwezo kwani vijana na kina mama watapata namna ya kujikimu kimaisha kwa kujiajiri wenyewe.
“Kama tunataka kupunguza umaskini katika kaunti, ni lazima tuhakikishe kuwa kina mama na vijana wameimarika kiuchumi na hii inawezekana kupitia hazina kama ya uwezo,” aliongezea Ngunjiri.
Ngunjiri alimalizia kwa kusema kuwa hazina ya uwezo inaweza kubadilisha maisha ya vijana na kina mama wengi iwapo pesa wanazopokea zitatumiwa vizuri kwa kuwekezwa katika miradi inayoweza kurejesha pesa hizo.