Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kaunti 19 zinazokuza zao la pareto zimehimizwa kuwaunga mkono wakulima wa pareto ili kuimarisha zao hilo.

Meneja mkurugenzi wa shirika la Highchem Agriculture, Dkt Wachira Maina amesema ingawa baadhi ya kaunti zimenunua mbegu za kusambazia wakulima, mengi zaidi yanahitajika kuafanywa ili kurejesha ukuzaji wa pareto katika hali yake ya hapo awali.

Akizungumza kwenye idara ya kukagua mradi wa Pareto katika eneo la Tetu Subukia siku ya Jumatatu, Dkt Maina alisema sekta ya pareto imekuwa ikikumbwa na changamoto mbalimbali kama vile kutozwa kodi ya juu, pamoja na ukosefu wa soko la kimataifa kutokana na hatua ya kutosajiliwa.

Maina alisema kuwa iwapo changamoto hizo zitashughulikiwa, wakulima wengi huenda wakakumbatia kilimo cha pareto.

Mkurungezi huyo alisema kwamba kutokana na ukosefu wa malipo kutoka kwa iliyokuwa bodi ya pareto nchini (Pyrethrum Board of Kenya) ambayo kwa sasa inafahamika kama Kampuni ya kutengeza pareto (Pyrethrum Processing Company PPC), wakulima wengi wangali hawataki na pia wanahofia kujihusisha na kilimo cha pareto.

Hata hivyo, amesema kulegezwa kwa baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yanadhibitiwa na serikali kwenye sekta ya ukuzaji wa pareto utapelekea wakulima kukumbatia upandaji wa pareto.

Kulingana naye, ingawa kampuni ya High Chem ilianza kununua pareto kutoka kwa wakulima na kuitengeza, kwa sasa hakuna mikakati kabambe ambayo imewekwa kwa kuwa Kampuni ya kutengeza pareto ya PPC iko chini ya kitengo cha pareto na mimea mingine ya kiwanda (directorate of pyrethrum and other Industrial crops).

Wakati huo huo, Maina alisema kuwa tangu walipoanza kununua pareto, wamepata tani 152 za zao hilo kutoka kwa wakulima ambao idadi yao ni zaidi ya elfu sita.

Aliwahimiza wakulima kupanda zao hilo akisema wanatumai sekta hiyo itaimarika na kunawiri tena.

Kando na hayo, Maina alisema wanawapa wakulima motisha ili waweze kurejelea kilimo hicho kama vile kupitia kwa njia ya kuwapa mbegu za pareto, huku gharama ya mbegu hizo ikitozwa kutoka kwa malipo yao.

Baadhi ya wakulima wa pareto waliohojiwa na wanahabari wamekumbatia hatua hiyo ya kulegezwa kwa baadhi ya mambo yaliyokuwa yamedhibitiwa na serikali kwenye sekta ya pareto, wakisema kuwa hatua hiyo itawafaidi pakubwa kwa kuwa watapata malipo bora kutokana na zao hilo.

Wakulima hao walidokeza kuwa serikali ya kitaifa na zile za kaunti zinafaa kuwaunga mkono wakulima wa zao la pareto kikamilifu ili kuhakikisha hitaji la pareto kwenye soko linaaafikiwa.