Mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa ulioidhinishwa na serikali ya Kaunti ya Mombasa katika ruwaza yake ya mwaka wa 2035, unaendelea kuibua hisia tofauti miongoni mwa viongozi wa kaunti hiyo.
Mgombea wa kiti cha ugavana Suleiman Shahbal ameshikilia kwamba mradi huo kamwe haufai kufanyika kwani utawaathiri kwa kiasi kikubwa wakaazi wa kaunti hiyo.
Akiongea mjini Mombasa, Shahbal alidokeza kwamba kuna njama fiche baina ya viongozi wa kaunti hiyo na wawekezaji wa kibinafsi wanaoufadhili mradi huo, na huenda wakaazi wanaoishi katika nyumba hizo wakalazimika kulipa ada za juu.
Haya yanajiri baada ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuwataka wakaazi wanaoishi katika nyumba hizo kukuu kuondoka ili kutoa fursa kwa ujenzi wa nyumba za kisasa.
Mradi huo wa mabillioni ya pesa umekuwa ukiibua hisia miongoni mwa viongozi wanaompinga Gavana Joho, huku wakidai kuwa kuna njama ya kuwauzia watu binafsi nyumba hizo za umma.