Shahidi mmoja amepata wakati mgumu kuelezea mahakama iwapo Shule ya msingi ya Star Of The Sea, jijini Mombasa ilihusika katika wizi wa mtihani.
Afisa wa upelelezi Edward Rono, kutoka kituo cha polisi cha Urban jijini Mombasa, alishindwa kufafanua iwapo mitihani waliyoinasa ilikuwa na nembo ya Baraza la mitihani nchini Knec.
Rono aliiambia mahakama kuwa hana ufahamu iwapo Waziri wa Elimu Fred Matiang'i alitangaza kuwa hakukuwa na visa vya wizi wa mitihani katika eneo zima la Mombasa.
Siku ya Jumatano, Rono alisema kuwa walifanikiwa kunasa karatasi tatu za mitihani katika mtandao wa kijamii wa Whatsapp.
“Tulinasa karatasi za somo la Hesabu na Kiengereza zote zikiwa katika kundi la kijamii lifahamikalo kama 'The star family' kwenye simu za walimu wa shule hiyo,” alisema Rono.
Afisa huyo pia alishindwa kuelezea iwapo aliweza kulinganisha nambari za siri za mitihani waliyoinasa na ile iliyofanywa kwa wakati huo.
Rono alikuwa akitoa ushahidi wake kwenye kesi ya wizi wa mitihani inayowakabili walimu 12 wa shule hiyo, walionaswa mwezi Novemba mwaka jana.
Ikumbukwe kuwa Waziri Matiang'i alisema wazi kuwa hakuna visa vya udanganyifu wa mitihani ulioshuhudiwa katika shule za Kaunti ya Mombasa., licha ya shule hiyo kuhusishwa na wizi huo.
Kesi hiyo itaskizwa Novemba 21, mwaka huu.