Jengo la Mahakama ya Mombasa. [Picha/ thekenyatoday.com]
Shahidi mmoja kwenye kesi ya kupinga ushindi wa mbunge wa Likoni Mishi Mboko amesema kuwa zaidi ya mawakala 10 wa chama cha Jubilee walizuiliwa kuingia ndani ya vituo vya kupigia kura katika uchaguzi wa Agosti 8.Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na aliyekuwa mbunge wa Likoni Masoud Mwahima, alisema kuwa uchaguzi huo haukuwa wa uwazi na haki.Akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Erick Ogola, Masoud Mwalim Ndoro, ambaye alikuwa wakala mkuu wa chama cha Jubilee Kaunti ya Mombasa aliiambia mahakama kuwa uchaguzi huo haukuwa wa haki na uwazi, kufuatia hatua ya mawakala wa Jubilee kuzuiliwa kuingia katika vituo cha uchaguzi.“Uchaguzi wa Agosti 8 eneo bunge la Likoni haukuwa wa uwazi na huru kwa mujibu wa katiba,” alisema Ndoro.Akitoa ushahidi wake siku ya Jumatatu, Ndoro alisema kuwa ilimlazimu kuingilia kati ndiposa mawakala hao wakubaliwe kuingia ndani ya vituo hivyo.Ndoro alitoa mfano wa kituo cha Vijiweni na shule ya msingi ya Shika Adabu.“Ilinilazimu kuingilia kati ndiposa wakakubaliwa kuingia ndani ya vituo hivyo ingawa zoezi la kupiga kura lilikua tayari limeanza,” alisema Masoud.Wiki iliyopita mahakama hiyo ilidinda kutupilia mbali kesi hiyo licha ya Mishi Mboko kuwasilisha ombi la kutaka kesi hiyo kutupiliwa mbali kwa kusema haikuwa imetimiza vigezo vya sheria za uchaguzi.Akitoa uamuzi huo siku ya Jumatano, Hakimu Erick Ogola alisema kuwa hakuna sababu kuu zilizowasilishwa mbele ya mahakama ambazo zingesababisha kesi hiyo kufutiliwa mbali.Jaji Ogola alisema kesi hiyo imetimiza vigezo vyote vya kesi za uchaguzi kwa mujibu wa katiba.“Vigezo na kanuni zote za kesi za uchaguzi zimezingatiwa kwenye kesi hii, kinyume na inavyodaiwa na Mishi Mboko,” alisema Ogola.