Thomas Mutua, afisa kutoka Idara ya madini, Kaunti ya Mombasa, ameelezea mahakama kuwa meli iliyozamishwa baharini ilikuwa imebeba kemikali ya kutengeneza mbolea wala sio dawa za kulevya.
Mutua aliambia mahakama siku ya Jumatano kuwa kulingana na ripoti ya uchunguzi wa mahabara, ni wazi kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba kemikali aina ya 'gypsum', ambayo hutumika kutengeneza mbolea.
Mutua ni shahidi wa pili kuambia mahakama kuwa meli hiyo haikuwa imebeba heroini bali mbolea.
Mwezi Aprili, mtafiti kutoka mahabara ya serikali Joram Wambua, aliambia mahakama kuwa waligundua madini ya 'gypsum' walipofanya utafiti wa kemikali zilizopatikana ndani ya meli ya MV Darya.
Wambua aliongeza kuwa hana ufahamu kuwa meli hiyo ilikuwa na heroini.
Itakumbukwa kuwa mkuu wa polisi wa kituo cha Kilindini Simon Simotwa, aliiambia mahakama kuwa yeye pamoja na wenzake waliikagua meli hiyo kwa mara ya kwanza iliposhikwa baharini ila hawakupata dawa za kulevya.
Kesi hiyo inawakabili raia tisa wa kigeni kutoka Pakistan na India, na watatu kutoka Kenya, wanaodaiwa kunaswa na dawa za kulevya Bandarini Mombasa zenye thamani ya shilingi bilioni 1.3.
Meli hiyo ilizamishwa baharini na serikali mwezi Agosti 29, 2014 baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa agizo la kuchomwa kwa meli hiyo.
Kesi hiyo itasikizwa tena Septemba 14, mwaka huu.