Mwakilishi wa kina mama katika Kaunti ya Nairobi Bi Rachael Shebesh ametoa wito kwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero kutafuta suluhu ya kudumu kuhusu mzozo unaoshuhudiwa baina ya maafisa wa kaunti na wahudumu wa matatu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akiongea katika shule ya mtakatifu Clevers jijini Nairobi baada ya kuyakabidhi makundi ya kina mama na vijana pesa za kuendeleza miradi ya maendeleo, Shebesh alisema kuwa ipo haja ya serikali ya Kaunti ya Nairobi kuwahusisha wadau wote wa sekta ya matatu katika jitihada zake za kutafuta suluhu ya kudumu katika sekta ya uchukuzi.

“Namuomba Gavana Kidero kufanya mazungumzo na wahudumu na wamiliki wa magari ya uchukuzi na pia kuwahusisha wabunge kusuluhisha mzozo huu,” alisema Shebesh.

Kauli ya Shebesh inajiri huku serikali ya Kaunti ya Nairobi ikishikilia kuwa ni sharti magari yote yasio na leseni ya kuegesha katikati mwa jiji la Nairobi kukamatwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Aggrey Adoli, kutoka afisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi, alizitaka Kamati zinazosimamia mpango wa kiusalama wa Nyumba Kumi kueleewa sheria kikamilifu ili kuepuka kutatua maswala ambayo yangefaa kushughuklikiwa na mahakama.

Adoli alisema kuwa imebainika kuwa baadhi ya wanachama wa kamati hizo kwenye vijiji mbalimbali wanajaribu kutatua mizozo ikiwemo ubakaji ambayo haiko chini ya mamlaka yao.

“Sio kila kitu kitatatuliwa kwa kuwepo maelewano. Iwapo kuna jambo linalofaa kufikishwa mahakamani basi ni sharti liwasilishwe.Tunaelewanaje hata kama ni maswala ya ubakaji, mauaji na hata ukandamizaji wa watoto wachanga?” aliuliza Adoli.