Huku mvua kubwa ikizidi kushuhudiwa katika sehemu mbalimbali humu nchini, serikali ya kaunti ya Nakuru imejipanga vilivyo kukabiliana na athari hizo.
Kwa mujibu wa Gavana Kinuthia Mbugua,shilingi milioni 12 zimetengwa kwa ajili ya kukabiliana na mafuriko katika sehemu mbalimbali.
Alikuwa akizungumza mjini Nakuru wakati wa kikao na wanahabari Jumanne.
"Tunaona athari za mvua hii na ndiposa kama serikali ya kaunti ya Nakuru tumetenga shilingi milioni 12 kwa ajili ya kukabiliana na swala hili," alitoa wito kwa viongozi kutoingiza siasa katika swala hill kwani ni mkasa na athari wala sio kujiimarisha kisiasa.
Kwa mujibu wa Gavana Mbugua, fedha hizo zilikuwa miongoni mwa zile zilizotengwa kwa ajili ya El-nino.
Itakumbukwa kuwa mvua inayoendelea kwa sasa imewahangaisha wakaazi katika maeneo ya Nakuru mjini Magharibi.