Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Muungano wa 'Sisterhoods Of Kenya' (AOSK) kwa ushirikiano na tume ya haki na amani ya jimbo katoliki la Nakuru CJPC imezindua mashindano ya uandishi wa insha miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi, upili na katika vyuo vya kidini kama njia ya kueneza amani nchini.

Mada ya insha ya wanafunzi wa shule za msingi ni ‘Nina uwezo wa kubadilisha na kuunganisha Kenya’, huku ya wanafunzi wa shule za upili ikiishia kwa maneno ‘......Umoja ni nguvu, Kenya yenye umoja inaanza nami', huku ile ya wanafunzi walio kwenye vyuo vya kidini ikiishia kwa maneno ‘......kueneza usawa wa kijinsia ni wajibu wangu'.

Siku ya mwisho ya kuwasilisha insha hizi ni mnamo 30 mwaka huu ambapo mwanafunzi atakayeibuka bora katika shindano hili atazawadiwa shilingi elfu sita, huku wa pili akizawadiwa shilingi elfu nne naye wa tatu atazawadiwa shilingi elfu mbili.

Wanafunzi wote watakaoshirikia katika mashindano hayo watatuzwa vyeti vitakavyokuwa na kauli mbiu ya siku ya kitaifa ya wanawake duniani ambapo shindano hilo lilizinduliwa.

Mtawa Temba, ambaye ni afisa wa usawa wa kijinsia katika Tume ya Haki na Amani ya jimbo katoliki la Nakuru, alisema lengo la kuwepo kwa mashindano haya ni kuwapa vijana nafasi ya kujihusisha kwenye harakati za kueneza amani na usawa.

Kila mwaka wakati wa kuadhimisha siku ya wanawake duniani, mada tofauti hutolewa kwa mashindano ya uandishi wa insha.