Shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za binadamu la Huria, limeanzisha mradi unaolenga kuwasaidia vijana wanaorandaranda mitaani mjini humo ili kuwalinda dhidi ya unyanyasaji wanaopitia mikononi mwa jamii.
Akizungumza na mwandishi huyu afisini mwake siku ya Alhamisi, meneja mratibu wa shirika hilo, Betty Sidi, alisema kuwa wanalenga kutumia mradi huo kuwasaidia zaidi ya vijana 200 wenye talanta ikiwemo kuwaunganisha na wahisani ili kuwapa fursa ya kujiendeleza kimasomo.
“Vijana wengi wanaorandaranda mitaani wana vipaji na talanta ambazo zikitambuliwa na kukuzwa wataweza kujitegemea na kurejea hali yao ya kawaida. Kama Huria tunalenga kuhakikisha kuwa hili linatekelezwa,” alisema Sidi.
Aidha, afisa huyo alisema kuwa mradi huo pia unalenga kupunguza visa vya vijana wanaorandaranda mtaani kujiunga na makundi ya uhalifu kama al-Shaabab, hasa baada ya utafiti uliofanywa na shirika hilo mapema mwezi huu kubaini kuwa wengi wa vijana hao wanasajiliwa na makundi yaliyoharamishwa.
Sidi vilevile alihimiza jamii kukoma kuwatenga na kuwadhulumu vijana hao na badala yake kuwapa wosia na usaidizi kando na kulinda haki zao za kikatiba.
Kwa muda sasa, vijana wanaorandaranda mitaani mjini Mombasa wamelalamikia kuhangaishwa na maafisa wa polisi mjini humo kwa madai ya kuwa wao ni wezi.