Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini Haki Afrika limedhihirisha wasiwasi wake kufuatia ongezeko la visa vya dhuluma za kijinsia katika Kaunti ya Mombasa.
Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Khalid Hussein amesema kwamba shirika hilo linapokea aghalabu kisa kimoja cha dhuluma kila siku kinyume na hapo awali ambapo ni kisa kimoja au viwili vilivyokuwa vikiripotiwa katika afisi za Shirika hilo kwa wiki, hali inayoashiria wazi kwamba visa vya dhuluma za kinyumbani vimeongezeka.
Akizungumza mjini Mombasa katika Afisi za Shirika hilo siku ya Ijumaa, Hussein ameitaja hali hiyo kama inayohitaji kutatuliwa kupitia kwa ushirikiano kati ya viongozi wa kidini, mashirika ya kijamii na wataalam wa ushauri katika kaunti hiyo ili dhuluma hizo zidhibitiwe.
Mtetezi huyo wa haki za kibinadamu vile vile amesema kwamba kumekuwepo na vitisho kutoka kwa wafungwa waliyohusika katika dhuluma hizo za kinyumbani ambao mara kwa mara huwapigia mashahidi katika kesi hizo na kuwatishia, na akasema kwamba shirika hilo linashirikiana na idara ya usalama na ile ya magereza ili kuwakabili wahalifu hao.
"Tunashangazwa na jinsi hali ilivyo kwa sasa mjini Mombasa, visa vya dhuluma za kijinsia vimeongezeka mno ikilinganishwa na hapo awali na hali hii imetokana na wazazi wenyewe kutowaripoti wahusika kwa maafisa wa polisi ili hatua za kinidhamu zichukuliwe kikamilifu," alisema Khalid.
Hisia za Khalid zinajiri baada ya tukio la hivi majuzi ambapo mwanamke mmoja alimchoma mumewe hadi akafariki kisha akamuua mtoto wake na kumzika kisiri katika eneo la Likoni mjini Mombasa.