Baada ya feri moja kukwama katika kivuko cha Likoni siku ya Alhamisi na kuzua taharuki kivukoni humo, hatimaye Shirika la huduma za feri KFS, limejitokeza kuomba msamaha.

Share news tips with us here at Hivisasa

KFS, kupitia mtandao wao wa Facebook, ilisema kwamba hali hiyo ilisababishwa na hitilafu ambapo mashine ya chombo hicho ilikwama na kusababisha feri hiyo ya MV Kwale kupoteza mwelekeo.

Shirika hilo limeomba msamaha kwa wote walioathiriwa na tukio hilo lililochukua takribani saa nzima, na kusema kwamba ni hali iliyokuwa nje ya uwezo wao.

“Tungependa kutangaza kwamba hakuna majeruhi walioripotiwa katika kisa hicho. Hilo ni tatizo la kimitambo tu na wataalam wetu wanalishughulikia,” KFS iliandika.

Wakati huo huo, wamewashukuru abiria hao kwa kuwa wavumilivu wakati wa zoezi la kuwasaidia kutoka katika feri hiyo na kuvuka ng’ambo ya pili.

“Kweli tunasikitishwa na tukio hilo lakini tungependa kuwashukuru abiria wote kwa kuwa wavumilivu na pia kutuelewa wakati huu ambapo vyombo vyetu mara nyingine vina shida.”