Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya St. Joseph’s Thim ilioko eneo la Maseno, Kaunti ya Kisumu ambayo inadhaminiwa na Kanisa la Got Calvary Legion Maria, watafaidika na msaada wa vipatakilishi shuleni mwao.
Got Calvary Legion Maria Church kwa ushirikiano na Shirika la Kijamii la Panama Community Bassed Organisation, (PCBO) katika eneo hilo kupitia kwa mdhamini wake mkuu Reagan Oscar wa Uingereza, Shule hiyo itafaidika na msaada wa vipatakilishi tano kufikia mwezi Julai mwaka huu.
“Tukishirikiana na Kanisa la Got Calvary, tunataka kuwahakikishia hawa makinda wetu hali nzuri ya masomo na teknolojia ili waweze kufikia viwango vya kisasa katika kushindana na wenzao na kutamba katika ulimwengu huu wa kidijitali,” alisema Oscar.
Mdhamini huyo mkuu alisema hayo siku ya Jumatatu kwenye mkutano ambao uliandaliwa katika ofisi kuu ya Kanisa hilo ilioko mjini Kisumu.
Aidha Oscar alisifia kazi nzuri inayofanywa na walimu wa shule hiyo ambao wamewezesha wanafunzi hao kuelewa tarakilishi kwa kushirikisha somo hilo kwenye silabasi zao.
St. Joseph ambayo iliasisiwa mnamo 2011 ikianza na chekechea imetimu katika kiwango cha darasa la pili mwaka huu na inaendelea kumiminikiwa na wanafunzi wapya kila mwaka kutokana na somo hilo kushirikishwa shuleni humo.
Wanafunzi wote wa shule hiyo kuanzia kwa wale wa chekechea wana uwezo wa kufungua tarakilishi na hata kuitumia kuandika na kusoma.