Shirika la Kulinda Mashahidi nchini – WPA, linaendelea na mikakati ya kufungua afisi jijini Kisumu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa Mkuu wa Uhusiano Mwema kwenye Shirika hilo Calvin Oredi, alisema kuwa afisi hiyo itafunguliwa hivi karibuni, ili kuwahudumia wakazi wa Magharibi ya nchi.

Kwenye mahojiano ya kipekee na na mwanahabari wetu jijini Kisumu Jumanne alasiri, Oredi alisema wanalenga kuleta huduma zao karibu na wananchi, hasa wale wasiokuwa na uwezo wa kusafiri hadi jijini Nairobi.

“Tunaendelea kusambaza huduma zetu kote nchini ili kuwafikia wakenya wengi wanaohitaji huduma. Kando na ofisi zetu za Nairobi, tuko mbioni kufungua afisi katika miji ya Kisumu na Nairobi hivi karibuni,” alisema Oredi.

Shirika la kulinda Mashahidi nchini, lilibuniwa mwaka 2008 na hufadhiliwa na serikali.

Licha ya ufadhili huo, shirika hilo huendesha masuala ya kuwalinda mashahidi kwa njia huru, pasina kuingiliwa na yeyote serikalini au nje ya serikali.

Shirika hilo hushughulikia mashahidi kwenye kesi zinazohusiana na ugaidi, wizi wa mabavu, unajisi, ubakaji, mauaji, ufisadi na dhuluma za kijinsia.

Mashahidi ambao hulindwa ni kama vile watoto, wahanga wa dhuluma za kimapenzi na kijinsia, wazee na wagonjwa.

Mtu yeyote ana haki ya kutuma maombi ya kuhusishwa katika mpango wa ulinzi wa mashahidi.

Mashahidi hulindwa kutumia mbinu mbali mbali, ikiwemo kuhamishwa hadi maeneo salama, kutumia majina bandia na vikao vya kesi kuandaliwa faraghani.